HII NI MAITI YA NANI!!!!!
Nilipokuwa mwanafunzi wa sekondari,
niliwahi kushuhudia mwili wa mwanafunzi mwenzetu ukigombewa na wazazi
wake. Huyu mwanafunzi mwenzetu alifariki ghafla shuleni na ikabidi
wazazi wake wafahamishwe ili waseme maiti isafirishwe kwenda wapi.
Mama
alisema, maiti ya mwanaye ibaki hapo alipofia, kwani atakuja kuichukua
na kuisafirisha kuipeleka kwao (mama) kwa mazishi. Baba naye alisema
hivyo hivyo. Walimu wakaamini kwamba, baba na mama wanazungumza jambo
lilelile. Lakini walipowasili pale shuleni, ndipo walipogundua kwamba,
hawakuwa wanawasiliana na watu walio pamoja.
Baba alikuwa na dini
nyingine na mama alikuwa wa dini nyingine na walishaachana kitambo.
Tangu walipoachana wazazi hawa, kila mmoja akawa anamvutia mtoto aingie
au afuate dini yake. Kwa jinsi tulivyokuwa tunamfahamu marehemu,
hakuwa hasa mtu wa dini fulani. Wakati wa vipindi vya dini, huyu
mwenzetu alikuwa anaingia mara kwenye madarasa ya waislamu, mara
wakristo na alikuwa anaingia kwenye madhehebu mbalimbali.
Basi,
wazazi hawa walikuwa kila mmoja akitaka kuchukua mwili wa marehemu.
Kila mmoja alikuwa akitoa maelezo ni kwa nini yeye ndiye anayestahili
kumzika mtoto kwa dini yake. Malumbano haya yalikuwa makubwa mpaka
vyombo vya dola vikahusishwa. Nakumbuka alikuja afisa mmoja wa
upelelezi kwenye malumbano hayo. Katika kujaribu kutafuta muafaka,
afisa huyu alizungumza kama vile kwa kuhutubia akisema: " Inasikitisha
kwamba, kijana wetu mpendwa, anaingizwa kwenye choyo na ubabe wa
kuoneshana nani zaidi, katika hali hii ambapo hawezi kujitetea.
Naamini, huyu marehemu kwa sasa anawachukia wazazi wake wote, kwani
anajua wazi hakuna anayempenda hata mmoja, bali wanatumia kifo chake
kama uwanja tu wa mapambano ya kujitosha kwao.
Naamini, hivi sasa
marehemu angeombwa kuchagua rafiki na ndugu wa kweli, angechagua
wanafunzi wenzake na walimu wa dini. Hii inatokana na ukweli kwamba,
hawa hawakutaka kumpangia aabudu au kuifuata imani gani ya dini.
Tunaambiwa aliingia kwa waislamu, na aliingia kwa wakristo pia,
hakuzuiwa au kusemewa, alikuwa huru.
Kuwa na dini ni kuwa na
uhuru. Kuwa na dini ni kuwapa wengine uhuru wa kuwa wao. Kuwa na dini
siyo kutumia tatizo la mwingine kujifaharisha, kuonesha ubabe na
urijali ulionao. Hiyo ni kibri ambayo kwa mtu aliyepoteza mwili kama
huyu kijana wetu anaiona na kuijua vizuri, haipendi hali hii..."
Hotuba
hiyo ilisaidia sana, kwani hatimaye ndugu wa upande wa mama na wale wa
upande wa baba walikaa chini wakiwa na adabu mpya na kujadili.
Hatimaye walikubaliana kijana azikwe kwa dini ya mama yake.
Miaka
30 baadaye, nakutana tena na watu wanaogombea maiti, watu wanaoamini
kwamba mzoga wa binadamu una maana yoyote. Sijawahi kuona mtu akitoa
shati au gauni kwenye mfuko wa nailoni na kuvaa mfuko huo badala ya
kuvaa shati au gauni, nimesema sijawahi kuona, huko ni kujidanganya.
Nimekuwa nikiona sana jambo hilo, ambapo ni pale watu wanapogombea
mwili.
Inaonesha wazi kwamba, binadamu bado ni mjinga sana juu
ya maisha yake. Mwili, mwili ni nini, na hadi wapi? Kama mwili ungekuwa
na maana sana, baada ya mtu kufariki usingekimbizwa mochuari,
usingepakwa asali au usingechomwa sindano ili usiharibike na kuleta
usumbufu wa harufu na maradhi. Mwili siyo mimi wala wewe. Mwili
haujawahi kuwa mwenye mwili na hautakuja kuwa. Mwili ni kama tochi tu,
ambayo umeiazima ili iweze kukusaidia kufika kijiji cha pili, kutokana
na giza na njia ya uchochoro ambayo unatakiwa kuipita ili kufika kijiji
hicho cha pili. Mwili ni kifaa na siyo wewe, bali wewe unakitumia
kifaa hicho Binadamu anajibainisha kwenye maisha haya ya hapa duniani
kupitia mwili wake, lakini yeye siyo mwili.
Mwili ni ubainisho,
ni chombo cha kutumika kwa kusudi la kidunia tu. Baada ya muda mwili
hukoma kuwepo, hujimaliza wenyewe au kumalizwa, ili binadamu amudu
kuingia hatua nyingine ya maisha ambayo haitumii au haihitaji mwili.
Tangu ulipozaliwa umeoneshwa na kufundishwa kwamba, wewe ni mwili kwa
njia zote. Akili yako imeshika kutu kwa kuamini kwamba, mwili ni wewe
na wewe ni mwili. Huna uwezo tena wa kuuona ukweli, kwa sababu vipimo
vyako vyote kuhusu maisha vinaishia kwenye akili, ambayo nayo pia
haikuhusu, siyo yako, umepachikwa tu.
Kwa ujinga huu wa kutojua
mwili ni nini na sisi ni nani, ndipo ambapo tunaingia kwenye ujinga wa
kuendeshwa na miili yetu, hisia zetu na akili. Kila mmoja anaamini
kwamba, mwili wake ukipotea, ukishindwa kutumika, yaani akifa, basi huo
ndiyo mwisho wake. Kama hiyo ni kweli, ina maana binadamu hana maana
kabisa, ni upuuzi usiofaa kuelezewa!
Yaani binadamu amekuwepo
ili awepo kwa mwezi mmoja, miaka kumi, hamsini, sabini, tisini, au mia
tu. Halafu baada ya hapo basi. Huu ni uongo mkubwa sana, unaoweza
kukubaliwa na akili makapi ya kulishwa tu! Anayetafakari zaidi kidogo,
atabaini kwamba, mwili ni mwili tu, ni kasha tu.
Ni kasha ambalo
muda wake wa kutumika ukiisha mtumiaji au [wewe] analiacha kwa sababu
haliwezi kukidhi kile anachokihitaji hapa duniani. Mtumiaji anachukua
kingine ambacho kinakidhi wakati huo [baada ya kifo]. Kwa hiyo,
binadamu hafi bali mwili ndiyo unaofikia ukomo wa muda wake wa matumizi
kwa sababu mbalimbali. Anapokufa John au Hamisi, haina tofauti.
Anapokufa mkulima hohehahe au tajiri kuliko wote duniani, pia haina
tofauti. Wote wanapita kwenye hatua muhimu ya mabadiliko, ambapo
wanaacha matumizi ya kifaa kilicho kuwa ndicho pekee kinachoweza
kuwabainisha na wengine hapa duniani na kuchukua kingine ambacho
hakiwezi kuwabainisha tena na wale wenye miili bado.
Anapokufa
John au Hamisi, haijalishi kama amezikwa kwa jeneza la dhahabu na
mizinga 100 au kwa masululu butu na kaniki. Kuzikwa ni utaratibu wa
kimazoea wa kuhifadhi mwili ambao sasa ni mzoga tu, ili usisumbue watu
wengine kwa harufu na maradhi. Kuzika haina maana kwamba, kunambadili
aliyekuwa akitumia mwili huo [marehemu], la hasha. Kama unadhani kwamba
Mungu anahesabu umezikwa na dini gani, umezikwa na shehe au padri
gani, ndiyo afanye uamuzi wa kukupokea mbinguni au hapana, ujue
unahitaji msaada wa haraka, kama siyo kupelekwa milembe. Ujue hujui
chochote ingawa umekuwa ukujidanganya kwamba unajua.
Mungu wa
kweli hahangaiki na mzoga, bali sisi kwa ufinyu wetu ndiyo tunaodhani
kwamba, mizoga au[maiti] hii ina maana. Mara nyingi nimekuwa
nikiwaambia jamaa zangu, ‘nikifa, mtaangalia ni mazingira gani ni
rahisi kwenu kuutupa au kuuhifadhi mwili wangu. Kwa nini? Kwa sababu,
kama sikuwa karibu na Mungu wakati nikiwa na mwili, huo, ukaribu
utaletwa leo wakati nimeupoteza mwili huo kwa sababu tu, mwili wangu
umezikwa kwa dini ya babu yangu? Ukosefu wa ufahamu wa kiwango kikubwa
sana. Kama nilikuwa karibu na Mungu wakati wa uhai wangu, basi hata
nikitupwa ****** baada ya kufa, ukaribu huo hautakufa. Mungu hayatazami
mambo kama Abdallah Juma au John Maiko! Kwani kuzika hasa ni kitu
gani?
Hatuziki watu ili waende mbinguni. Kama ni hivyo,
wanaoliwa na wanyama, kuungua na kuteketea kabisa, wao Mbinguni
hawatafika? Kama hawatafika, watahukumiwa vipi siku ya mwisho? Mwili
hautakiwi Mbinguni, hauna kazi huko, kwani huko siyo makazi ya miili.
Mwili unafaa tu duniani Kuna zile jamii ambapo mtu akifa mwili wake
huchomwa moto na kuteketezwa kabisa Unadhani hizi jamii hazimjui Mungu
kama wewe unavyomjua? Zinamjua, tena pengine vizuri zaidi yako. Lakini,
zimeng’amua kwamba, mwili ni kasha tu, likishindwa kufanya kazi, ni
sawa na taka nyingine, hutupwa dampo na kuteketezwa kwa moto. Mtu
akishauacha mwili wake [kufa] hana tena uhusiano na mwili huo. Mtu huyo
anakuwa ameingia kwenye awamu nyingine ya maisha ambayo haihitaji mwili
na ambayo haihitaji kujua huo mwili umezikwa na nani na wapi. Ni akili
isiosogea ndiyo ambayo inashindwa kufanya mikokotoo midogo kama hii.
Ukiona
watu wanagombea maiti, jua kwamba, hata kama wamevaa masuti na
kubandika digrii zao kwenye kila ukuta, ni watoto wadogo kiufahamu.
Ukiona mtu pia anaacha wosia mrefu wa namna anavyotaka akifa azikwe,
naye huyo ni mpujufu tu wa ufahamu. Kwa nini? Unagombea kuuzika mwili wa
fulani ili upate kitu gani, ili huyo marehemu naye apate nini? Hata
usipouzika, kumbuka kwamba, ameshakufa na ukiuzika, ameshakufa pia.
Haifanyi tofauti yoyote kwa kweli. Kama nilivyosema awali, huuziki mwili
ili uende Mbinguni kwa sababu mbingu haiko ardhini. Unaufukia ili
usisumbue kwa harufu.
Ukienda kwenye nchi zenye vita hasa vya
wenyewe kwa wenyewe, utagundua kirahisi kwamba, maiti hana maana, maiti
ni msumbufu kwa kunuka na kusambaza magonjwa. Tunazika kwa sababu tuna
nafasi ya kuhifadhi mwili kwa heshima na taratibu ambazo zinaonesha
kujali mwili wa mwenzetu ambao ulitumika kufanya mema au maovu. Kwenye
kizuizi na misukosuko au vita, hakuna anayeweza kukumbuka, siyo kuzika
bali hata kufukia maiti. Kila mmoja anafikiria kuendelea kubaki na mwili
wake kwanza. Aliyepoteza wake, basi hakuna anayemjali, kwani haina
maana kabisa kumjali. Hata aina nyingine za mazishi
zinaonesha tu ujinga na utoto wa binadamu.
Mazishi ya
kifahari yenye kuhusisha majeneza ya dhahabu
na vyakula na vinywaji vya bei mbaya. Ni ujinga uliopindukia kwa
sababu, inawezekana kabisa marehemu au wanaotoa fedha hizo hawajawahi
kumsaidia aliye hai hata kwa chupi ya mguu. Sasa kusaidia huo mzoga kwa
mapambo inaongeza kitu gani? Nimesema unapoona mtu anaacha wosia ili
azikwe vipi, wosia ambao wakati mwingine ni kero tupu, ujue huyo naye
ni mtoto wa miaka sita, bila kujali anamiliki au amesoma hadi kiwago
gani. Ni utoto kwa sababu, unapoacha mwili, siyo kazi yako kusema huo
mwili ufanyiwe kitu gani. Waliobaki, wanaweza kuamua kuuchoma mishikaki
[kama wanakula watu], wanaweza kuukausha na kuuweka kwa maonesho,
wanaweza kuufukia kwenye kijishimo cha futi tano na ukafukuliwa na fisi
usiku, na wanaweza kuuzika kwa matarumbeta na sanduku la dhahamu. Ni
hiari yao. Ukishauacha mwili huna mamlaka nao tena.
Ni wale
waliobaki ndiyo wanaolimbuka nao tu. Nimekuwa nikitazama hii tabia ya
kugombea maiti kwa jicho lenye mashaka na ufahamu wa binadamu, hofu
zake na ufisadi wa nafsi alionao. Mtu amekufa, wewe unasema nataka
nimzike mimi, sawa. Kwani mbona huendi hospitalini ukaulizia maiti
ambazo hazina ndugu na kuzichukua ili ukazizike? Wewe si unapenda
kuzika na unaamini kumzika mtu kwa dini yako ni jambo kubwa na la maana
sana? Pia hospitalini, utapewa maiti nyingi zisizo na ndugu.
Ukishazipata zibadili majina na kuziingiza kwenye dini yako kwa mujibu
wa utaratibu wa dini yako. Halafu zika! Hiyo huitaki kwa sababu haina
maslahi, haina kuonesha ubabe ambao umefundishwa na wazazi, na jamii na
pengine hata na dini yako hiyohiyo. Kugombea maiti ni kujiogopa.
Kugombea
maiti ni kujitafuta kimakosa. Kugombea maiti ni kutojua dini. Kugombea
maiti ni kudhani mtu anaweza kuwa na uhuru wa kuwa mtu mwingine.
Kugombea maiti ni kufikiri wewe ni mwili, Kugombea maiti ni njaa ya
mali au haja ya kupanda kithamani. Kwa ujumla ni ubabe wa kimtaa zaidi.
Mara nyingi imeshatokea, anapookotwa maiti na watu wakaanza kuulizana,
jamani maiti hii ni ya nani? Ujue maiti hiyo itazikwa na serikali.
Hakuna mtu au kundi la kidini la eneo hilo ambalo litajitokeza
kuichukua na kuizika maiti hiyo kwa imani yake. Hilo haliwezekani kwa
sababu halina utamu.
Halina kubishana, halina kulumbana, halina
ujuaji na ubabe. Anasubiriwa mtoto mwenye mzazi walioachana na walio na
dini tofauti. Huyu akifa, hasira na visasi vyote vya nyuma vinaishia
kwenye mwili wake. Atasubiliwa yule ambaye alishakuwa kwenye dini yetu
akatoka, huyo akifa
tuna sababu ya kugombea maiti. Kama nilivyosema,
hapo kuna malumbano na ujuaji na kuoneshana. Halafu bado mnajiita
mnatumikia dini, zipi? Ni ujinga tu.