MAUMIVU ya tumbo ni tatizo linaloweza kumpata mtu yeyote, mwanamke au mwanaume, mkubwa au mdogo. Maumivu haya husumbua kwani huwa hayaishi, yaani yanatulia kwa muda flani na kurudi tena, aina hii ya maumivu pia inaweza kuwa ya moja kwa moja, yaani hayatulii na wakati mwingine mgonjwa hupata nafuu kwa kujikunja au kushikilia tumbo.
Maumivu yanaweza kuwa upande wa juu wa tumbo au upande wa chini na yanatulia kwa vipindi na kurudi yakiwa makali au madogo lakini hayaishi.
JINSI TATIZO LINAVYOTOKEA
Kama tulivyoona, humtokea yeyote mwanamke au mwanaume, utokeaji wake hutofautiana kwa jinsi. Kwa mwanaume vyanzo vya maumivu haya vinaweza kuwa hernia au ngiri au matatizo kwenye korodani, lakini kwa wote vyanzo vinaweza kuwa vidonda vya tumbo, matatizo ya mkojo, kidole tumbo, matatizo ya utumbo mkubwa, kukosa au kufunga kupata haja kubwa, gesi kujaa tumboni. Yapo mengine kama kuwa na mawe kwenye mfumo wa mkojo au kifuko cha nyongo, matatizo ya ini na mengineyo.
Matatizo mengine yanayoweza kuleta maumivu haya ni mchafuko wa tumbo kwa kula vyakula au kunywa vinywaji vyenye sumu au vichafu, hali hii inaweza kuambatana na kutapika au kuharisha.
Kwa upande wa wanawake, matatizo hutokea zaidi chini ya tumbo na huhusisha kibofu cha mkojo kama ilivyo kwa wanaume, mfuko wa uzazi, mirija ya uzazi na vifuko vya mayai.
Kuharibika kwa mimba au mimba kutunga nje ya kizazi ni sababu kubwa ya maumivu ya tumbo kwa wanawake walio katika umri wa kuzaa, lakini hali hii huambatana na kutokwa na damu ukeni, kwa mama mjazito maumivu ya tumbo inaweza kuwa matatizo katika mimba na kama anakaribia kujifungua basi ni uchungu.
Magonjwa yanayosababishwa na maumivu haya hutofautiana kwa kiasi kikubwa kuanzia vyanzo hadi dalili.
Vyanzo vya matatizo katika sehemu ambazo magonjwa yanatokea yanaweza kuwa maambukizi (infections), uvimbe, kuumia na athari zitokanazo na madawa, vinywaji, vyakula kama tulivyokwishaona hapo awali na hata kuumia iwe kwa ajali au upasuaji.
Kwa upande wa wote wanawake na wanaume, ugonjwa huambatana na dalili mbalimbali, mfano kwa mwili kudhoofika, kupoteza hamu ya kula na hata kupoteza hamu na uwezo wa kufanya tendo la ndoa.
Wanawake ndiyo waathirika wakubwa wa tatizo hili la maumivu kwa kuwa wana viungo vingi katika mfumo wa uzazi. Matatizo katika viungo hivyo ni kama vile maambukizi ndani ya kizazi yanayotokana aidha na utoaji wa mimba au maambukizi ya ukeni. Maambukizi haya huweza kusambaa hadi katika mirija ya uzazi na kuathiri mfumo wa uzazi. Uwepo wa uvimbe katika viungo vya uzazi vya mwanamke mfano uvimbe wa ‘fibroid’ au aina nyinginezo, huweza kusababisha maumivu ya daima au ya kuja na kupotea.
Tatizo hili linahitaji uchunguzi wa kina kwani athari kubwa ni kupoteza uwezo wa kushika ujauzito.
DALILI ZA TATIZO
Kama tulivyoona hapo awali, dalili za tatizo hili hutofautiana kati ya mtu na mtu hata kijinsia.
Mtu mwenye vidonda vya tumbo hulalamika maumivu ya tumbo juu ya kitovu ambayo husambaa hadi mgongoni na huambatana na kiungulia au moto kifuani, mtu mwenye matatizo ya ini, tumbo huuma sana upande wa kulia kwa juu na wakati mwingine tumbo hujaa au kuvimba.
Matatizo katika njia ya mkojo huambatana na maumivu chini ya tumbo yanayozunguka upande wa ubavu wa kulia au kushoto, maumivu ya mkojo au kutoa mkojo wenye rangi ya njano kila siku.
Kwa ugonjwa wa kidole tumbo au ‘Appendicitis’, maumivu huwa chini ya tumbo upande wa kulia usawa wa kati ya kitovu na nyonga ya kulia.
Maumivu yanayohusiana na viungo vya uzazi vya mwanamke huwa daima chini ya kitovu na yanaweza kusambaa kulia na kushoto, wakati mwingine huambatana na kutokwa na uchafu au damu ukeni, maumivu wakati wa tendo la ndoa au wakati wa hedhi. Maumivu haya ni vema yakaangaliwa kwa kina kwani yanaweza kuwa makali na ghafla mfano mimba kutunga nje ya kizazi au kidole tumbo.
UCHUNGUZI, TIBA NA USHAURI
Maumivu ni kitu kigumu kwani tiba bila kujua chanzo chake huwa ngumu, uchunguzi wa tatizo hili la maumivu hutegemea historia ya mgonjwa na aina ya maumivu. Vipimo vinavyoshauriwa ni kama vile; vipimo vya damu, haja kubwa, ultrasound, X-ray na vingine ambavyo daktari wako ataona vinafaa. Ni vizuri kutopendelea kunywa dawa za kutuliza maumivu bila kujua hasa chanzo cha tatizo.
Ni vizuri sana ukafanyiwa vipimo katika hospitali kubwa za wilaya na mikoa.