Recent Posts

PropellerAds

Tuesday, February 13, 2018

Mtoto ni nani?

 Mtoto ni nani? 
Sheria na mikataba mbalimbali inayozungumzia huduma na haki za mtoto, inamtambulisha mtoto kama mtu yeyote mwenye umri wa miaka chini ya 18. Hata hivyo, kutumia umri kama msingi wa tafsiri ya utoto hakuwezi kutusaidia kujua kwa nini mtu mwenye umri huo aitwe mtoto. Katika makala haya, ningependa tumtazame kwa nini? Watoto wapewe Mafundisho ya Mungu.
Mitazamo mbalimbali ya dhana ya utoto
Moja kabisa, kuna mtazamo wa ukuaji. Hali ya ukuaji wa mwili inayosababisha mabadiliko yanayoendana na upevukaji, mabadiliko ya homoni, uelewa wa mtu na kadhalika huweza kuchukuliwa kama kigezo cha kumtofautisha mtoto na mtu mzima. Mtoto tunamtazama kama mtu mwenye viungo viteke vinavyoendelea kukua, wakati mtu mzima ni yule asiyefikia kimo cha upevukaji. 

Mabadiliko yanayoongoza ukuaji wa mtoto yanaweza kupimwa na njia za kisayansi ili kuelewa maendeleo ya jumla yanayofanana kwa watoto wote bila kujali wanakoishi na athari nyinginezo za kimakuzi. Ingawa kigezo hiki hakizingatii ukweli kwamba kila mtoto ni mtu tofauti na watu wengine wa umri wake, bado kwa kutumia wastani wa yale yanayoonekana kuwa ‘kawaida ya watoto wa umri fulani,’ tunaweza kuwachukulia wengine wenye tofauti na kawaida hiyo kuwa na ukuaji usio wa kawaida. 

Katika jamii nyingi za ki-Afrika kwa mfano, matukio fulani yanaweza kuchukuliwa kuwa mpaka wa utoto na utu uzima. Kuna mila kama jando/unyago, ndoa na kadhalika vinavyotazamwa kama kivuko cha utoto kwenda utu uzima. Pia zipo imani/mila za kidini zenye matukio ya namna hiyo kama kipaimara, sakramenti ya kwanza na kadhalika. Haya yote ni matukio yenye ‘uwezo’ wa kumvusha mtoto kwenda utu uzima bila kueleza ni mambo gani hasa yanamfanya mtu aonekane ni mtoto au mtu mzima.

Mitazamo ya Jamii kuhusu Mtoto.
Kwa ujumla tunaweza kusema mitazamo inayojaribu kumtambua mtoto inatofautiana na wakati mwingine kupingana kulingana na mahitaji ya anayetafsiri. Wakati sayansi inaweza kutupa sifa za mtoto pasipokujali amekulia katika mazingira gani, jamii  nayo inaweza kuja na tafsiri yake inayoendana na mazingira yake kumwumba mtoto. 

Yapo mazingira ambayo mtoto huonekana  kama mtu asiye na hatia na ambaye hukosea kwa kutokuelewa. Kwamba utoto ni umri wa kutokuhukumiwa kwa matendo yake na hivyo ni wajibu wa jamii kumlinda mtoto na mabaya ya watu wazima, kumsamehe anapokosea na kumrudisha kwenye mstari wa jamii kwa uangalifu ili hatima yake aishi kwa furaha na amani.

Lakini yapo mazingira ya kijamii yanayomtazama mtoto kama mtu anayezaliwa na uovu na uhalifu wa asili. Mtazamo huu ndio unaotufanya wakati mwingine tuamini kwamba watu wazima wanayo mamlaka ya kuwastaarabisha na kuwaadhibu watoto wanapokosea kwa sababu hukosea kwa makusudi shauri ya asili ya uhalifu iliyo ndani yao. Ubatizo wa watoto kwa baadhi ya imani za kidini ni mfano wa matambiko yanayokusudia kung’oa asili hii ya uovu inayoaminika kuambatana na mtoto tangu anapozaliwa.

Biblia inasema nini juu ya Mafundisho kwa watoto.

“Nanyi akina baba, msiwachokoze watoto wenu; bali waleeni katika adabu na maonyo ya Bwana” (Waefeso 6:4).
Hii inamaanisha kwamba wazazi wote lazima tuwalee watoto wetu katika kumfahamu Yesu Kristo kama Bwana na Mwokozi. Hili ni jukumu la kila mzazi ambaye ameokoka, kuhakikisha kwamba watoto wake wanajua njia ya wokovu jinsi Biblia inavyofundisha. Hili si jukumu lao tu, bali inafaa kuwa tamaa ya mioyo yao kwamba watoto wao wanaokoka. Je, hii ni tamaa juu ya maisha ya watoto wako? Je, katika mipangilio yako yote kuwahusu watoto wako, je wao kumjua Kristo ni tamaa na kusudi lako la kwanza? Je, wewe unatamani kwamba watoto wako waokoke au la? Kuwaongoza watoto wako ili waokoke, ndio maana ya adabu na maonyo ya Bwana.
Biblia inasisitiza sana kuhusu kuwalea watoto katika adabu na maonyo ya Bwana. Kwa mfano katika Kumbukumbu la Torati 6, tunasoma wakati Musa alikuwa amekaribia kufa na Waisreali walikuwa karibu kuingia katika nchi ya Kanani. Yeye Musa aliwakumbusha kuhusu sheria ya Mungu na kuwaelezea jinsi
walipaswa kuishi maisha yao katika nchi ya Kanani. Miongoni mwa mambo mengine yote, aliwasihi kwamba walihitaji kuwafundisha watoto wao sheria ya Mungu. Haikutosha tu kwamba wao waliijua na kutii, bali pia walihitaji kuwaeleza watoto wao kuhusu sheria hiyo. Walihitaji kuwafundisha watoto wao na wasisahau.
Hili jambo la kuwalea watoto katika adabu na maonyo ya Bwana ni jambo ambalo wakristo wengi hata katika historia wamelitilia mkazo sana. Wao wamekuwa waangalifu sana jinsi wamewalea watoto wao kwa utukufu wa Mungu. Kwa sababu ya umuhimu wa jambo hili, mahubiri mengi yamehubiriwa na vitabu vingi vimeandikwa kuhusu jambo hili.
·         kuwalea watoto katika adabu na maonyo ya Bwana ni jambo ambalo lipaswa kufanyika katika jamii na kufanywa na wazazi.
·         katika majuku yetu ya kuwalea watoto katika adabu na maonyo ya Bwana, tuhakikishe kwamba hatuwalazimishi watoto wetu kufanya uamuzi Fulani.

·         Biblia inatuonesha  jinsi  gani tunapaswa kuwalea watoto wetu katika adabu na maonyo     ya Bwana. Waefeso 6:4

mfundishe mtoto wako kujua neno la Mungu.

Tunafaa kuwa waangalifu sana katika  jambo hili maana roho ya motto ikipotea utadaiwa mzazi maana ni jukumu letu kama wazazi kuwahekimisha watoto wetu na kuwafundisha kwa upole na upendo wa hali ya juu.
   
 Usitaka kuwafanya wajue yale yaliyomo katika Tv na internet au Mambo mengine yasio na maana, badala yake wacha waijue Biblia. Huku ndiko kulea na kufundisha ambako Mungu aneheshimu na ambako kunaleta wokovu katika nafsi ya mtoto. Biblia inasema,
 “…kwa maana umeikuza ahadi yako, kuliko jina lako lote” (Zaburi 138:2). Mungu huwa anawabariki wote ambao wanaliheshimu neno lake miongoni mwa wanadamu wote.

Wafundishe kujua kwamba neno la Mungu ni chakula cha kila siku cha nafsi zao. Hi sasa haimaanishi kwamba wanapaswa kuona hii kama jukumu tu, kwa sababu jinsi wanavyoendelea kusoma Biblia indivyo watakapoendelea kujua Mungu na Roho Mtakatifu ndivyo atalavyoedelea kuwazungumzia kila siku kupitia kwa neno la Mungu.
Wafundishe kuomba vema

Maombi ni jambo ambalo linaazisha mabadiliko katika nafsi ya mwanadamu. Kazi ambazo tunafanya za hudumu haziwezi kufaulu bila maombi.

Maombi ni ishara kwamba mtu anaishi kiroho. Hii ndio ishara ya kwanza kwamba mtu kweli amezaliwa mara ya pili. “Bwana akamwambia, simama, enenda zako katika njia iitwayo Nyofu, ukaulize katika nyumba ya Yuda mtu aitwwaye Sauli, wa Tarso; maana, angalia, anaomba” (Matendo ya Mitume 9:11). Sauli alikuwa ameanza kuomba na hiyo ilikuwa ishara tosha kwamba alikuwa amebadilika. Maombi ndio ilikuwa ishara kati ya watu wa Mungu na wale ambao si Mungu; wanadamu walianza kuliita jina la Bwana (Mwanzo 4:26). 
   
Maombi ni chombo ambacho kinaleta ufanisi katika mambo ya kiroho. Ikiwa mtu anamaliza muda katika maombi, atapata kwamba mtu huyu atakua kiroho. Kwa hivyo ikiwa hatutajitahidi katika maombi, hatutakuwa jinsi tunapaswa kukua. Mkristo amabye anaendelea vyema kiroho ni yule ambaye anasoma neno la Mungu kila siku na analitii na pia ni yule anajitahidi katika maombi. Yeye huwa anaomba mengi na anapata mengi. Yeye kila wakati huwa anamwambia Yesu kila kitu na huwa anajua jinsi ya kutenda katika hali zote.

Mwatamani, wala hamna kitu, mwaua na kuona wivu, wala hamwezi kupata. Mwafanya vita na kupigana, wala hamna kitu kwa kuwa hamwombi”
              (Yakobo 4:2).

 Watoto wanapaswa kufundishwa utii kwa wazazi.
Hii ni amri ya Mungu ambayo amewaahidi wale wote ambao watatii,s kwamba wao watakuwa na maisha marefu (Kutoka 20:12). 
Katika  kitabu cha Waefeso  Biblia  inasema kwamba hii ndio amri ya kwanza ambayo iko  na ahadi. Hii inaonyesha kwamba Mungu amempa mzazi mamlaka ya kuhakikisha kwamba anamlea na kumfundisha mtoto mambo muhimu ya maisha. Kwa sababu hii, watoto wanapaswa kufundishwa kwamba ni Mungu ambaye amewaweka katika maisha na mikono ya wazazi wao. Pia wanapaswa kufundishwa kwamba kuwatii wazazi wao ni jambo ambalo Mungu anawaamru walifanya.
Biblia inafundisha kwamba, “Fimbo na maonyo hutia hekima; Bali mwana aliyeachiliwa himwaibisha mamaye” (Mithali 29:15). Kuhusu utiifu na upendo Biblia inasema, “Ni vema mwanadamu aichukue nira wakati wa ujana wake” (Maombolezi 3:27).
Watoto wanapaswa kufundishwa kuwaheshimu na kuwajali watu wote.

Katika kitabu cha Warumi tunasoma kwamba, “Pendo halifanyii jirani neno baya; basi pendo ndilo utimilifu wa sheria” (Warumi 13:10) na kwamba kila jambo linakamilishwa katika hili neno moja; upendo.  Huu ndio upendo ambao tunafaa kuwafundisha watoto wetu, kuwapenda na kuwaheshimu watu wote. Ikiwa tutawafundisha upendo huu, basi hiyo ndio itakuwa sheria ya kuwaongoza katika maisha yao yote.

Biblia inasema kwamba, “Basi yote yote mkatakayo mtendewe na watu, nanyi watendeeni vivyo hivyo, maana hiyo ndiyo torati na manabii” (Mathayo 7:12). Hivi ndivyo inapaswa kuwafundisha watoto wetu na tunafaa kuchunguza maisha yao kulingana na mstari huu. Tunafaa kuwasisitizia kwamba dini ya kweli inajumlisha kuwafanyia wengine mema
Pia tuwafundishe kuwapenda na kuwashughulikia wanayama wa wanyumbani kwa njia mzuri. Biblia inasema kwamba,
 “Mwenye haki huufikiri uhai wa mnyama wake”
           (Mithali 12:10).
Pia tukumbuke kuwafundisha kwamba hawafai kuwa watu wenye hasira,  badala yake tuwahimize kusaidia wengine katika yale ambayo ni mazuri kufanya. Tuwafundishe kuwapenda na kuwasidia wale ambao ni maskini. Mungu amesema katika neno lake kwamba amebarikiwa yule ambaye anawajali maskini, naye Mungu atamkumbuka siku ya taabu zake. Pia Biblia iansema kwamba yule ambaye anawahurumia maskini, huyu anamkopesha Mungu na kile ambacho amempa Mungu, atarudishiwa. Tunafaa kuwaonyesha kwa tabia yetu kwamba kweli sisi tunaamini ahadi hizi za Mungu. Tuwahimize watoto wetu kuwa na tabia ya kuwasaidia wengine kila wakati bila kukoma. Ikiwa watoto wetu tutawalea katika njia hii, basi tutakuwa tunawasaidia kufahamu na kuelewa ukristo wa kweli ni ukristo wa aina gani.


Watoto wanapaswa kufundishwa kuwa watu waaminifu.
Kuwa mwaminifu ni jambo la maana sana katika maisha ya mkristo. Ni jambo la huzuni sana kuona jinsi dhambi inavyojitokeza katika maisha ya watoto wetu. Biblia inasema kwamba kutoka katika tumbo sisi ni wenye dhambi na tunazungmza uongo (Zaburi 58:3). Kwa hivyo tunafaa kuwa waangalifu sana kuhakikisha kwamba watoto wetu wanajua ukweli wa neno la Mungu.
Wanafaa kujua kwamba wao ni wenye hatia machoni pa Mungu kwa sababu ya dhambi zao. Kwa sababu hii, tunafaa kuhakikisha kwamba hatuwaongozi watoto wetu katika dhambi. Tuhakikisha kwamba hatuwaogopeshi au hatuwalazimishi katika jambo, kwa sababu hii inaweza kuwafanya wadanganye kwa sababu tunataka ukweli kutoka kwao. Pia tuhakikishe kwamba kabla hatujawaadhibu, tunafanya upelelezi wa kutosha ili tudhibitishe jambo kabla ya kufanya uamuzi wowote. 
 Kila wakati tuwakumbushe kuhusu kile ambacho Biblia inasema: “Aendaye kwa unyofu huenda salama; Bali apotoshaye njia zake atajulika” (Mithali 10:9). Kila siku usichoke kuwaonyesha uzuri na faida ya kuishi maisha amabyo ni ya uaminifu.
Biblia inasema kwamba, “Bali waongo, na wasioamini, na wachukizao, na wauaji, na wazinzi, na wachawi, na hao waabuduo sanamu, na waongo wote, sehemu yao ni katika lile ziwa liwakalo moto na kiberiti” (Ufunuo 21:8).
Watoto wanapaswa kufundishwa unyenyekevu.

Hili jambo ambalo tunajifundisha kutoka kwa Bwana wetu Yesu Kristo. Yeye Kristo hangenyenyekea, basi hangeweza kutuletea wokovu.  Biblia inasema kwamba, “Kumcha Bwana ni maonyo ya hekima; Na kabla ya heshima hutangulia unyenyekevu” (Mithali 15:33). Yule ambaye anajiinua yeye hunyenyekezwa na yule ambaye anajinyenyekeza huinuliwa na Mungu na wanadamu.

Kwa hivyo ili tuweze kuwasaidia watoto wetu, lazima tuhakikishe kwamba tunawaonya juu ya kiburi katika maisha yao. Kiburi ndicho kilisababisha Adamu na Hawa kuanguka katika dhambi. Kwa kawaida kila mwanadamu amezaliwa akiwa na kiburi kwa sababu sisi sote tumetoka katika Adamu. Lakini sasa hii haimaanishi tuendelee katika kiburi. Biblia inatuambia kwamba tuepuke dhambi, tuache dhambi. Tuwafundishe watoto wetu kuwa wenye unyenyekevu na kuwaheshimu watu wote.

Pia wanafaa kuhimizwa kwamba hawapaswi kuwa wenye kiburi kwa wale ambao ni wa mri wao. Lakini tuwafundishe kunyenyekea hata wakati mwingine kukubali kudharauliwa kwa ajili ya amani. Wanapaswa kuheshimiana na wale ambao ni wa umri wao na kuwaheshimu wote. Ninajua kwamba haya yanaonekana kuwa mambo magumu kwao, lakini ukweli ni kwamba haya ndiyo mambo ambayo yanapaswa kuzingatiwa na wanadamu wote ikiwa wanataka kuishi maisha ya amani na watu wote.

 Rafiki, tunatakiwa kuwapa watoto kipaumbele nyumbani kwetu na kanisani kwetu. Tunatakiwa kufanya kila tuwezalo ili kuwaelekeza kwenye njia sahihi, na si kuwaelekeza upotevuni. Je, utajitoa kulipatia suala hili umuhimu? Pengine utazawadiwa kuwa na mtazamo wa kitoto zaidi, ule wa kuwa na imani ya kawaida!

Nyumba nyingi zinaharibika kwa sababu ya ukosefu wa nidhamu kwa watoto katika nyumba hizo. Ikiwa mkulima anatarajia mazao mazuri, ni lazima ahakikishe kwamba kila wakati analichunga shamba lake na anang’oa magugu ambayo yanajitokeza kila mara katika shamba hilo. Asipofanya hivi, basi ni wazi kwamba yeye hataona mazao mazuri katika shamba hilo. Kwa hivyo mzazi anaweza kuweka nidhamu mzuri katika nyumba yake, lakini asipokuwa makini kuondoa tabia mbaya, hasira na dhambi miongoni mwa watoto wake, basi ni wazi kwamba hatakuwa amesaidia sana watoto wake. Yeye anaweza kuwa mchungaji mzuri na baba mzuri lakini asipokuwa mfalme katika nyumba yake, mambo mengi yataenda vibaya sana. Ikiwa akina baba watapuuza majukumu yao ya kuwalea watoto wao katika nidhamu na maonyo ya Bwana, basi wao wasitarajie watoto wao kukua katika njia za Bwana na katika nidhamu mzuri. Ikiwa katika nyumba nidhamu haifuatiliwi kikamilifu, kwa mfano ikiwa wakati fulani baba ni mwangalifu sana katika mambo ya nidhamu na wakati mwingine kwa sababu hataki watoto wamwogopi, anapuuza nidhamu hiyo, basi atapata kwamba pole pole atakuwa anapuuza majukumu yake kwa watoto wake na watoto wake watamzoea hivyo na itakuwa vigumu sana kuwaongoza vyema.