Mwigizaji maarufu Zsa Zsa Gabor amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 99.
Mumewe wa sasa Frederic von Anhalt amesema mwigizaji huyo alifariki baada ya kupatwa na mshtuko wa moyo akiwa amezingirwa na marafiki na jamaa.
"Kila mtu alikuwa hapo. Hakufariki akiwa peke yake,"
Alitengeneza zaidi ya filamu sita lakini alijulikana zaidi kwa kuwa na wanaume wengi na kupenda almasi.
Kwa hesabu zake mwenyewe Zsa Zsa Gabor aliwahi kuolewa mara nane na nusu, hakuchukulia ndoa yake kwa Mhispania mwaka 1983 kuwa ndoa kamili.
Alikuwa maarufu kwa miongo kadhaa, kabla ya hata kuibuka kwa Paris Hilton au Kim Kardashian.
Mwanamke aliyeshambuliwa mtandaoni ajitetea
Akitoa maoni juu ya kushindwa kudumu katika ndoa Gabor alisema katika ndoa zake alifanywa kama msimamizi wa nyumba kwa sababu kila alipokuwa akipewa talaka yeye aliachiwa nyumba.
Zsa Zsa Gabor alizaliwa mjini Budapest nchini Hungary tarehe 6 Februari 1917 na akahamia Marekani wakati wa Vita Vikuu vya Pili vya Dunia.
Aliigiza filamu yake ya kwanza Hollywood mwaka 1952.
Aliigiza zaidi ya filamu 70, lakini alifahamika sana kwa maisha yake ya kifahari.
Aliolewa mara ya kwanza akiwa na miaka 20 na ndoa yake iliyodumu muda mrefu zaidi ilikuwa yake ya mwisho alipokuwa na miaka 70 kwa Frederic von Anhalt.
Gabor alitawazwa Miss Hungary mwaka 1936, lakini baadaye akapokonywa taji hilo kwa kuhadaa kuhusu umri wake ndipo aruhusiwe kushiriki shindano hilo.
Aliigiza karika filamu maarufu kama vile Moulin Rouge (1952), Lili (1953) na Queen of Outer Space (1958). Hivi karibuni, aliigiza katika filamu ya Nightmare kwenye mwendelezo wa filamu za Elm Street na pia kwenye filamu za ucheshi za Naked Gun.
Mtoto wake wa pekee ni Constance Francesca Hilton, ambaye alimzaa na tajiri wa mahoteli Conrad Hilton. Alizaliwa mwaka 1947.
Mamake wakati mmoja inadaiwa alimwambia: "Si lazima umuoe mwanamume yeyote unayefanya mapenzi naye."
Gabor alisema alikuwa anaoa kwa sababu hakuwahi "kuacha kuwa Mkatoliki moyoni."
Kwenye kitabu chake kuhusu maisha yake alichokiandika mwaka 1993 kwa jina "One Lifetime is Not Enough", alidai kwamba alibikiriwa na Kemal Ataturk, mwanzilishi wa taifa la sasa la Uturuki, alipokuwa na miaka 15.
Alieleza kwamba alikuwa pia na uhusiano na nyota wa filamu za James Bond Sean Connery na Frank Sinatra, kando na msururu wa wanaume alioolewa nao.
Alidai kwamba aliwakataa John F. Kennedy na Elvis Presley.