l
Hapo zamani za kale katika nchi moja Afrika, paliishi mama mmoja
ambaye alikuwa mjane. Muda mfupi tu kabla ya mumewe kufariki walijaliwa
mtoto mmoja wa kiume ambaye huyo mama alimlea kwa shida na taabu nyingi.
Hata hivyo mama na mtoto wake walipendana ipasavyo. Hapo katika kijiji
chao kulikuwa pia na tajiri mmoja ambaye alikuwa bahili na katili kweli.
Yule kijana maskini alikwenda kwa tajiri kuomba kazi. Tajiri alimwambia
kwamba alikuwa na kazi kwake na angemlipa vizuri sana.
Kijana alifurahi kusikia hivyo na akamwuliza tajiri kwa furaha.
"Kazi gani hiyo utanipa mheshimiwa? Mimi nitaifanya vizuri mpaka hata wewe utafurahia."
Tajiri akamwambia, "Ukilala katika maji baridi sana usiku mzima,
nitakupa shillingi laki moja." Ulikuwa wakati wa baridi sana kwamba maji
ya ziwa karibu yagandamane kuwa theluji kwa baridi.
Lo! Kijana hakufikiria angeweza kuwa na pesa nyingi hivyo katika
maisha yake. Tamaa ya kutaka kumsaidia mama yake ambaye wakati huo
alikuwa mgonjwa na mzee, ilikuwa kubwa sana kwa hivyo akakubali bila
kufikiria. Mama aliposikia habari hizo karibu azimie kwa wasiwasi na
huzuni.
"Mwanangu sitaki uhatarishe maisha yako kwa sababu ya pesa. Mungu
yuko nasi na hajatuacha hata siku moja tukalala njaa. Atazidi kufanya
hivyo hivyo. Je, ukifa nitabaki na nani mwanangu? Mimi mzee sasa wala
sijiwezi!" Kijana alimjibu,
"Mama usiwe na wasiwasi wala woga wo wote! Nitaweza kabisa kulala
kwenye maji baridi mpaka asubuhi na siwezi kufa" Mama bado alizidi
kubisha, lakini kijana alisisitiza kabisa kwamba lazima afanye hiyo kazi
ambayo itawaondolea shida zote za kifedha, kama alivyoona yeye.
Kwa huruma ya mama na wasiwasi juu ya mtoto wake, alikwenda karibu na
ziwa pale alimotumbukizwa mtoto wake kwenye maji baridi kama barafu,
Alimwona kichwa tu kimelea juu ya maji. Mama aliwasha moto mkubwa karibu
na ziwa lile kwenye ufa, ili aweze kumwangazia angalao mwangaza na
kumwona. Usiku kucha mama mtu hakufunguka jicho hata dakika moja.
Alimlilia Mungu amtunze mwanae asife kwa baridi.
Kwa huruma ya Mwenyezi Mungu, kijana alistahimili baridi yote ile mpaka alfajiri siku ya pili.
Alikwenda kwa tajiri kupokea malipo yake lakini tajiri akamwambia.
"Hupati hata ndururu ng'o!"
"Kijana alishangaa akamwuliza, "Kwa nini mheshimiwa? Uliniahidi
kunipa shillingi laki moja nikilala katika maji yabaridi usiku mzima.
Usiku mzima nilikuwa ndani ya maji hayo na shahidi wako wameshuhudia na
pia mama yangu."
"Ehe, hapo sasa umenena. Mamako aliyekuwashia moto ili upate joto
usiku mzima. Hayo ndiyo yalikuwa maagano yetu? Sikumbuki tukiagana
kwamba mama yako atakuja na kuwasha moto mkubwa wa kukupa joto kisha
unidanganye umelala kwenye maji ya baridi. Unaniona mimi bwege sio?
Nenda zako, sikulipi cho chote."
Kijana alikasirika kweli na akamweleza jirani yake mzee Abunuasi.
Kama kuna watu Abunuasi aliowazira, ni matajiri waliopenda kuwaangamiza
maskini badala ya kuwasaidia. Abunuasi akamwambia kijana asiwe na
wasiwasi kwamba rafiki yake Sultan atamsaidia. Akamwambia aende kwake na
kumweleza habari zote. Kijana alifuata ushauri wa Abunuasi, lakini
Sultani aliposikia kisa chote kutoka pande zote mbili aliamua kwamba
kijana asipate malipo kamwe. Abunuasi alishangaa na uamuzi huo wa
Sultani mzima wa nchi akamwambia kijana bado asiwe na wasiwasi atapata
hela zake. Kijana alimwahidi Abunuasi kumpa shillingi elfu ishirini
akimsaidia.
Abunuasi aliandaa karamu kubwa na akawaalika watu wengi pamoja na
Sultani na yule tajiri pia. Alichinja mbuzi akatayarisha vitu vyote,
mchele, mboga zikakatwakatwa na kuwekwa kando. Moto mkubwa uliwahswa na
kila kitu kikawekwa kando ya moto, nyama ya mbuzi katika sufuria pamoja
na vitunguu na viungo. Mboga, mchele, zote zikawekwa kando ya moto na
Abunuasi akaenda kuwakaribisha wageni wake. Wageni walingojea chakula
siku kutwa hawakuona hata maji ya kunywa. Abunuasi aliwaambia kwamba
chakula bado kinapikwa jikoni na wala hakijawa tayari. Itabidi wangojee.
Mwisho walikasirika na kuingia wote katika jiko. Walikuta moto unawaka
vizuri na kando ya huo moto chakula chote walichokuwa wakikingojea kiko
kando ya moto huo mkubwa. Sultani akiwa mmoja wa wale waliokuwa na njaa
alisema.
"Abunuasi wewe akili zako zinafanya kazi? Hiki chakula ulisema
kinapikwa? Mbona moto uko kando na chakula kando? Hakitaiva hata baada
ya miaka elfu. Wewe mwehu kweli kama watu wanavyokusema. Unatulisha njaa
siku nzima?"
"Usiwe na wasiwasi Sultan, chakula kitaiva tu! Subira huvuta kheri mheshimiwa."
"Acha upuzi na ubwege. Hiki chakula hakitaiva kamwe. Hakipati hata joto la moto huo hata kama mkali kiasi gani"
"Kwa nini kisiive mheshimiwa? Wewe uliamua kesi ya kijana maskini
asilipwe na huyu tajiri nduli alipomlazimisha kulala kwenye maji baridi
usiku mzima. Kwa njaa na umaskini wake, alikubali. Naye mama yake kwa
upendo wa mwanae, alilala kando ya ziwa akimumlikia mwanae ili apate
kumwona tu kama angali hai. Wewe uliamua asilipwe kwa sababu ya huo
mwangaza aliyemlikiwa na mamake. Basi na hiki chakula kutokana na uamuzi
wako lazima kiive hivyo hivyo moto ukiwa kando." Sultani aliona aibu
kweli mbele ya watu hao wote, na akaamuru tajiri amlipe kijana pesa zake
mara moja na Sultani akampa Abunuasi zawadi kubwa kwa sababu ya ubusara
wake. Baada ya hayo yote kukamilika, chakula kiliwekwa juu ya moto,
kikaiva na wote wakala.
Wote walimshukuru Abunuasi sana!
Habari kubwa Magazetini Kenya leo January 22, 2024
-
Good Morning Mtu wangu wa nguvu kutoka Tanzania January 22,
2024,nakukaribisha kutazama kile kilichoandikwa katika kurasa za mbele na
za nyuma Magazetini...
6 hours ago