Shirika la Datang Telecom
International Technology Company Limited la Serikali ya China lina
mpango wa kujenga kiwanda kikubwa cha kutengeneza vifaa vya mawasiliano
kwa ushirikiano na Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL).
Rais wa
Shirika hilo Yuan Yong ametoa kauli hiyo mapema wiki hii baada ya
kukutana na kufanya mazungumzo na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania Samia Suluhu Hassan Ikulu jijini Dar es Salaam.Yuan Yong amemweleza Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan kuwa serikali ya China pia ina mpango wa kuikopesha Kampuni ya simu Tanzania (TTCL) kiasi cha shilingi bilioni 600 ili kuipa uwezo wa kiteknolojia na kupanua mtandao wa mawasiliano katika maeneo mbalimbali nchini humo hasa maeneo ya vijijini.
Rais huyo amesema lengo la mkakati huo ni kuifanya TTCL kuwa kampuni bora inayotoa huduma za mawasiliano kwa njia ya kisasa kuliko kampuni yeyote katika ukanda wa Afrika Mashariki na kati.
Amesema kuwa uhusiano mzuri kati ya Tanzania na China ndiyo uliosababisha shirika hilo kuweka mikakati ya kuwekeza katika sekta ya mawasiliano ili kuhakikisha wananchi wa Tanzania wanapata huduma bora za mawasiliano mijini na vijijini kwa njia ya kisasa bila usumbufu wowote.
Kwa upande wake, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, ameonyesha kufurahishwa na mikakati hiyo na kusisitiza kuwa serikali ipo tayari kwa uwekezaji huo mkubwa kwa ajili ya manufaa ya wananchi wa pande hizo Mbili.
Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan amesema ana imani kubwa kuwa uwekezaji huo ukikamilika utaiwezesha (TTCL) kufanya kazi kwa ubora wa hali ya juu kwa kutumia teknolojia ya kisasa.
Makamu wa Rais amesema serikali ya awamu ya tano imedhamiria kuelekea katika uchumi wa viwanda kwa kishindo hali ambayo itasaidia taifa kuongeza pato lake la taifa pamoja na kutoa ajira kwa mamia ya wananchi kupitia viwanda ambavyo vitajengwa nchini.
Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan, pia amepongeza mpango wa shirika hilo la mawasiliano la serikali ya China wa kutoa mafunzo mbalimbali kwa wafanyakazi wa TTCL ikiwemo ujenzi wa kituo kikubwa cha utafiti wa mawasiliano hatua ambayo itasaidia kuimarisha utendaji kazi kwa wafanyakazi wa TTCL ili waweze kuingiliana na teknolojia ya kisasa ya mawasiliano duniani kupitia tafiti zitakazofanywa Tanzania.