1. Mwanaume Kicheche:
Hakuna
mwanamke anayependa kuchezewa na wanaume, labda tu kama anafanya hivyo
katika juhudi zake za kujikwamua kiuchumi, lakini pale mwanamke
anapokuwa katika harakati za kutafuta mwanaume ambaye kama mambo yakiwa
mazuri wafunge ndoa, ni vyema akajiepusha na wanaume vicheche
wanaotongoza wanawake kwa lengo la kustarehe na kumaliza matamanio yao
ya ngono. wakati mwingine mwanaume mwenye tabia ya kuchezea wanawake
anaweza kumfuata mwanamke ambaye ametamani mwili wake na kujifanya eti
amebadilika na kuwa mtakatifu. Anaweza kujiweka katika mazingira
yanayoonyesha kwamba amebadilika ili kumvuta mwanamke. Shituka mwanamke,
jasiri haachi asili atakutumia kama condom na kisha kukutupilia mbali.
Wanaume wenye tabia hizo ni vigumu kubadilika. Inahitaji subira ya hali
ya juu kujiridhisha kama kweli amebadilika au anazuga ili apate
anachokitaka.
2. Mwanaume asiye na kazi na asiyejishughulisha:
Mwaume
asiye na kazi na asiyejishughulisha ni mzigo usio na mwenyewe. Mwanaume
asiyejishughulisha eti kwa sababu hajapata kazi huyo hana malengo.
Kukubali kuwa na uhusiano na mwnaaume wa aina hiyo ni sawa na kuishi na
mtu mfu anayetembea (dead alive), labda tu kama atakupa sababu
inayoingia akilini kuhusu kutokuwa kwake na kazi na kutojishughulisha
kwake. Kama atakuwa ni mtu wa kulalamika tu kwamba hakuna ajira na
haonyeshi dalili zozote za kuhangaika kutafuta hata vibarua ili kujikimu
eti kwa sababu ni msomi na badala yake anageuka kuwa ombaomba kwa ndugu
zake na marafiki zake Nawashauri wanawake muwaepuke wanaume wa aina hii
kwani hawafai wanataka kulelewa. Kama amekuona unafanya kazi au una
vibishara vyako vinavyokuingizia shilingi mbili tatu zinazokufanya uishi
vizuri hapa mjini jua kwamba hicho ndicho kilichomvuta kwako, ukikubali
umekwisha maana atakukamua hadi tone la mwisho kisha ahamie kwa
mwingine, si kilichomleta kwako hakipo, sasa awe na wewe kwa lipi....
3. Mwanaume asiyejiamini:
Kukubali
kuwa na mahusiano na mwanaume asiyejiamini ni sawa na kuishi na bomu
ndani ya nyumba. Mwanaume asiyejihisi kuwa yuko salama na mwenye mashaka
muda mwingi kuhusu uhusiano wenu, hutawaliwa na wivu wa ajabu ambao
licha ya kukuletea fedheha kwa ndugu, jamaa na marafiki zako, lakini pia
anaweza kukudhuru au hata kukutoa roho siku moja. Wanaume wasiojiamini
mara nyingi ni watu wa kujitilia mashaka kuhusu hali zao za kipato na
uwezo wao katika tendo. Kuwa na mahusiano na mwanaume asiejiamini
inabidi uishi kwa akili na uchague maneno ya kuzungumza kila uwapo naye,
kwani kila neno utakalotamka litatafutiwa tafsiri na kitakachofuata ni
tafrani, sasa tabu yote ya nini..... Tupa kule hafai kwa mchuzi wala kwa
kulumangia...
4.Mtoto wa mama:
Inawezekana
mwanaume akalazimika kuishi nyumbani kwao kwa muda baada ya kumaliza
masomo au amepoteza ajira na akawa bado hajapata ajira au hajapata
shughuli ya maana itakayomwezesha kujitegemea, hii inakubalika. Hata
hivyo kama mwanamke anakutana na mwanaume ambaye anaishi na wazazi wake
na haonyeshi dalili za kutafuta kazi au shughuli yenye kipato
itakayomwezesha kuondoka hapo kwao na kujitegemea, usije ukajiingiza
katika uhusiano na mwanaume wa aina hiyo, itakula kwako, huyo ashakuwa
kupe na tegemezi, utakuwa ni mzigo wako na atakuganda kama luba na
kupoteza bahati ya kukutana na wanaume wenye mwelekeo wa maisha.
5. Mwanaume anayependa kutukuzwa kama mfalme:
Unaweza
kukutana na mwanaume aliyejipachika kibandiko ufalme ambaye anapenda
sana kuhudumiwa kama mfalme. Yaani anataka afanyiwe kila kitu, na
hajishughulishi kukusaidia kazi hata zile zinazotakiwa zifanywe na
mwanaume, yeye kazi yake ni kukaa sebuleni na kuangalia TV au kusoma
vitabu au magazeti huku akiagiza kila kitu asogezewe miguuni. Hawezi
hata kunyanyuka kufuata kitu anachotaka na badala yake ni kuamrisha
aletewe. Mwanaume wa aina hii ni wa kuepukwa kwani mwanamke kukubali
kuwa na uhusiano na mwanaume mwenye tabia za kupenda kutukuzwa kama
mfalme ni kutaka kuishi kwa msongo wa mawazo na jakamoyo na hivyo
kufupisha umri wako wa kuishi hapa duniani. Kinga ni bora kuliko tiba,
ukikutana na mwanaume wa aina hii chapa lapa hakufai..
6. Mwanaume mwenye utititri wa watoto kila kona:
Mwanaume
kuwa na watoto nje ya ndoa si jambo la kushangaza siku hizi, lakini
pale unapokutana na mvulana mwenye umri wa miaka 25 lakini ana watoto
watatu kwa mama tofauti, mh! hapo sikushauri ujiingize kwenye uhusiano
na mwanaume huyo. Hata hivyo si lazima awe na miaka 25 tu hata mwanaume
mwenye umri mkubwa zaidi ya huo halafu ana watoto watatu au hata wanne
au zaidi kutoka kwa mama tofauti ni wa kuepuka. Hivi atakupa sababu gani
zilizomfanya akawa na watoto kwa mama tofauti kila kona ya mtaa mpaka
umuelewe! Kuwa na mahusiano na mwanaume aina hiyo ni kukaribisha shari
nyumbani kwako maana kila siku utapata wageni wanaokuja kudai hela za
matumizi kutoka kwa mumeo tena wengine watakuja kishari hasa na
kukuharibia siku. Mh mh! sikushauri mwanamke, sepa zako, bado nafasi
unayo ya kumpata mwanaume mwingine mwadilifu.
7. Mwanaume anayejipenda mwenyewe:
Mwanaume
anayejipenda mwenyewe ni kizungumkuti kingine ambacho wanawake
wanapaswa kujiepusha nacho. Utakuta mwanaume anajipenda mwenyewe hakuna
anachojali kuhusu mwenzi wake zaidi ya kujijali yeye mwenyewe. Wanaume
wenye tabia hii ya kujipenda wenyewe, huwa wana kawaida ya kujijali wao
wenyewe. Wanataka wavae nguo nzuri za thamani ili wao wapendeze na si
wenzi wao. Swala la kumjali mwenzi wake halipo katika vichwa vya wanaume
wa aina hii kabisa. Mwanamke sikushauri uingie katika moto huu.
8.Mwanaume bahili:
Unakutana
na mwanaume mtoko wa kwanza tu anakuchagulia aina ya chakula au
kinywaji kwa kuangalia bei rahisi na wakati wa kulipa anahesabia hela
yake mfukoni, huyo ni janga. Utakapoingia katika uhusiano na mwanaume wa
aina hii atakusumbua sana na pia katika kupanga bajeti nyumbani
usishangae akihesabu finyango za nyama au vipande vya samaki jikoni.
Sikushauri mwanamke, we ingia mitini hakufai huyo........
9.Mwanaume chapombe mlevi kupindukia:
Hakuna
ubaya mtu kunywa pombe, hasa kama unajua kiwango chako cha unywaji,
lakini kuwa na uhusiano na mwanaume mlevi anayekunywa pombe kupindukia
kila siku non stop 24/7 huyo hafai. Mwanaume wa aina hii ndio
wale wanaosema kunywa pombe watoto wakitembea uchi atajua mama yao. Hata
siku moja hawezi kuzungumzia maendeleo kwa ustawi wa familia, kwake
utakuwa ni msamiati mgumu.
10. Mwanaume mwenye kisirani :
Mwanaume
mwenye kisirani ni ngumu sana kuishi naye. Mwanaume mwenye kisirani na
anayependa kuweka vitu rohoni na asiyeweza kusamehe ni janga. kuishi na
mwanaume wa aina hii ni sawa na kuishi na explosive material ambayo
yakipata joto tu hulipuka. Mwanaume umetoka naye mtoko wa kwanza na kwa
bahati mbaya mhudumu wa mghahawa akasau kitu katika vitu mlivyoagiza
akagomba kupita kiasi na kuwakusanya mameneja wote wa mghahawa akiwemo
mpishi mkuu akilalamika. Na kama hiyo haitoshi mtaondoka hapo mghahawani
njia nzima kambeba kichwani mhudumu yule masikini aliyeghafilika mpaka
mwisho wa safari yenu na huenda akalala naye kichwani. Mwanaume huyo
hafai kama gome la mgomba lisilofaa kwa dawa ya miti shamba wala kuni,
labda kwa kufungia ugoro. Huyo mpishe ajiendee zake hakufai......