Recent Posts

PropellerAds

Tuesday, February 28, 2017

DAWA ZA NYWELE ZINAZOSABABISHA UVIMBE WA KIZAZI KWA WANAWAKE

Image result for women washing hair
Dawa za kulainisha nywele (relaxer) zimekuwa zinapendwa na wanawake wengi wa Afrika kwa kuwa zina uwezo wa kulainisha nywele na kumfanya apendeze na awe wa kuvutia.

Hata hivyo, wataalamu wa afya wanadai kuwa dawa hizo zinasababisha uvimbe kwenye kizazi kutokana na kemikali za dawa hizo ambazo huingia mwilini kupitia majeraha au ngozi wakati wa kupaka.

Daktari wa Manispaa ya Ilala, Laurent Chipata alifanya utafiti na kubaini kuwa dawa za nywele na vipodozi zina kemikali ambazo husababisha uzalishwaji wa vichocheo kwa kiasi kikubwa na kusababisha uvimbe kwenye kizazi uitwao fibroids au leimyoma.

“Kemikali hizi hupenya kwenye ngozi na wakati mwingine hata kwa harufu tu, husababisha kuzalishwa kwa wingi wa vichocheo aina ya estrogen ambavyo huchangia kuota kwa uvimbe wa fibroids,” anasema.

Dk Chipata anasema kukua kwa uvimbe kwenye kizazi hutokea katika kipindi ambacho mama yupo kwenye uzazi yaani kabla hajakoma hedhi.

Utafiti wa Dk Chipata ulifanywa nchini na kujumuisha wanawake wa kada tofauti tofauti wanaotumia dawa za nywele na wale wasiotumia na ukubwa wa tatizo hili ulibainika.

“Zipo kemikali tofauti tofauti zinazosababisha uvinbe kwenye kizazi, zipo za kwenye dawa za kilimo kama DDT na za kwenye mafuta ya ngozi kama vile mercury na hydroquionone,” anasema.

Dk Chipata anasema madhara yanayopatikana katika kemikali za vipodozi ni makubwa siyo tu kwenye kizazi bali nyingine husababisha saratani au kufeli kwa figo. Anatoa mfano wa kemikali ya zebaki (mercury).

“Dawa za nywele zina madhara si lazima zipenye kwenye ngozi baada ya mtu kupata jeraha la kuungua bali zinaweza kupenya zenyewe kwenye ngozi kutokana na mfumo wa ngozi,” anasema.

Anashauri kuwa ni vyema watu wakasoma kipodozi kimetengenezwa kwa nini kabla ya kukitumia na kuongeza kuwa ni salama zaidi kubaki na ngozi au nywele halisi badala ya kujibadilisha.

Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) imekataza vipodozi vyenye kemikali kama biothionol, hexachlorophene, mercury, vinyl chloride, zirconium na bidhaa zenye aerosol, chloroquionone, steroids, methylene na chloroform.
 
Image result for women washing hair
Utafiti mwingine uliofanywa mwaka 2012 na Dk Lauren Wise na wenzake nchini Marekani na kuchapishwa kwenye jarida la afya la nchini Marekani ulibaini kuwa vipodozi vingi vina kemikali zenye vichocheo vya estrogen ambavyo kwa kawaida huchochea kasi ya kuota kwa uvimbe kwenye kizazi cha mwanamke na wakati mwingine kwenye mji wa mimba. Kitaalamu uvimbe au vivimbe hivi hujulikana kama fibroids au myoma.

Dk Wise anasema aliwafanyia uchunguzi wanawake wanaotumia dawa za kulainisha nywele na kuangali umri walioanza kutumia dawa hizo, mara ngapi, waliungua kiasi gani na walikaa na dawa hizo kichwani kwa kipindi gani.

Aliwafuatilia wanawake 23,580 wanaotumia dawa za kulainisha nywele na baada ya kipindi fulani walipimwa. Kati yao, 7146 waligundulika kuwa na uvimbe kwenye kizazi baada ya kupimwa kwa mionzi na wengine kufanyiwa upasuaji.

Kwa nini relaxer ni hatari kwa wanawake?
Dk Wise anasema mchanganyiko ulio kenye dawa za nywele hasa zilizoandikwa “Lye Relaxer” ni sodium hydroxide wakati makopo ya dawa yaliyoandikwa “No Lye Relaxer” yana calcium hydroxide na guanidine carbonate.

Bidhaa za kulainishwa nywele zilizoandikwa ‘no lye relaxer’ zinadaiwa kusababisha majeraha kwa kiasi kidogo ukilinganisha na zile zilizoandikwa “Lye Relaxer”.