Wapo watu ambao ni waoga sana kuwajibika hasa linapokuja suala la
kufanya kile kitu wanachotakiwa kufanya. Utakuta ni watu wa kusingizia
sana hiki au kile, kwamba siwezi kufanya kwa sasa, kwa sababu hii au
ile.
Kwa mfano, utakuta mtu anataka kuanzisha biashara ya aina fulani, ambapo
ukiangalia kama ataanzisha biashara hiyo, itamsaidia sana mtu huyo
kuweza kuingiza kipato kikubwa na cha ziada.
Hata hivyo, kitu cha kushangaza au cha ajabu kwa sababu ya hofu ama
wasiwasi tu, mtu huyo atajikuta anatoa visingizio vingi sana mpaka
kushindwa kuanza biashara hiyo, ambayo ilitakiwa ainze mara moja.
Kitu usichokijua, kisaikolojia unaposhindwa kufanya jambo fulani kwa
sababu ya hofu za mara kwa mara, mawazo yako ya ndani, mawazo yanayoumba
au kupelekea mambo hutokea, huchukua hofu hiyo na kuihifadhi na
kuifanya kama ‘ulemavu’ wako.
Kwa hiyo kila unapojaribu kufanya jambo jipya utakuta wazo linashuka
haraka sana ndani yako, ‘Je ukishindwa itakuwaje? Si unaona wengi sana
huwa wanashindwa hapo,’? Utashangaa ubongo wako una hofu sana, hata
pengine bila kujua kwa nini?.
Lakini ukiangalia, hiyo yote inatokana na hofu ndogo ndogo ambazo
ulizibeba sasa zimekaa kwenye mawazo yako ya kina na imekuwa kama ndio
‘ulemavu’ wako wa kiakili yaani 'psychological disorders', sasa kila
kitu ukitaka kukifanya unakuwa una hofu.
Kitu cha kujiuliza kwa nini watu wanakuwa na hofu sana hasa pale wanapotaka kuanza jambo fulani? Chanzo hasa huwa nini?
Zifuatazo ni baadhi ya sababu zinazopelekea hofu moja kwa moja kwenye
maisha yako na kushindwa kuchukua hatua sahihi za majukumu yako.
1. Kuogopa kukosea.
Utakuta hapa hofu inazalishwa sana kwa sababu ya kuogopa kukosea.
Utakuta mtu anakuwa ana wasi wasi mwingi hivi jambo hili lisipokwenda
sawa itakuwaje? Mwisho wa siku kila kitu hufika mahali kimekwama.
2. Kuogopa kushindwa.
Pia kuna watu ambao wanajawa na hofu kwa sababu ya kuogopa kushindwa.
Kwa watu kama hawa kwao wanaona inakuwa ni bora wasifanye kabisa kuliko
wakafanya halafu wakashindwa. Kwa lugha rahisi watu wenye hofu hii huwa
hawafanikiwi.
3. Kutokujiamini.
Unaposhindwa kujiamini, elewa kabisa huwezi kufanikiwa katika kitu
chochote. Kujiamani mara nyingi ndio msingi wa mafanikio. Waangalie watu
ambao wanajiamini utakuta ni watu ambao wanamafanikio wakati
wasiojiamini hawana kitu maishani mwao.
4. Kuogopa ushindani.
Mwingine utakuta anashindwa kuanza jambo analotakiwa afanye, inaweza
kuwa biashara au kitu chochote eti kisa kwa sababu ya kuogopa ushindani.
Kwa jinsi anavyoogopa ushindani anajikuta hawezi tena kufanya kitu.
5. Kukosa hamasa.
Pia ni rahisi sana kuanza kuingiwa na hofu kama umekosa hamasa ya kile
unachokifanya. Ni muhimu sana kuwa na hamasa ili ikusaidie kukujaza
ujasiri wa kufanya hicho unachokifaya kwenye maisha yako.
6. Mawazo hasi.
Kama una mawazo sana kama vile ‘aah mimi sina uwezo wa kufanikisha hili,
huu mradi sio saizi yangu,’ uwe na uhakika hutaweza kufanya kwa
ujasiri, hapo utakuwa unajijaza hofu mwenyewe zitakazo kufanya ushindwe
tu.
Kimsingi, kuogopa kushindwa, kuogopa ushindani, kugopa kukosea, kukosa
hamasa, mawazo hasi na kutokujiamini ni moja ya sababu zinazokufanya
wewe uwe na hofu kubwa kwenye maisha yako.