Rais Kiir atatia saini mkataba huo jijini Dar es Salaam mbele ya mwenyeji wake, Rais wa Tanzania John Magufuli, ambaye kwa sasa ndiye mwenyekiti wa jumuiya hiyo.
Viongozi wa nchi za jumuiya hiyo waliidhinisha kukubaliwa kwa Sudan Kusini kujiunga na jumuiya hiyo kwenye mkutano mkuu uliofanyika mjini Arusha mwezi uliopita.
Sudan Kusini itakuwa nchi ya sita kujiunga na jumuiya hiyo iliyoanza kwa nchi tatu Tanzania, Kenya na Uganda. Rwanda na Burundi zilijiunga na jumuiya hiyo baadaye.
Baada ya kujiunga rasmi leo, Sudan Kusini inatarajiwa kufungua mipaka yake kwa ajili ya biashara. Tayari kampuni na asasi nyingi za kifedha kutoka Kenya zimefungua vbiashara nchini Sudan Kusini.
Wengi wanatarajia hatua ya leo itafungua fursa zaidi za kibiashara kati ya Sudan Kusini na nchi wanachama wa jumuiya.
Wadadisi wengine wanaamini kuwa baadhi ya miradi ambayo Sudan Kusini ingetaka kujumuishwa katika Jumuiya ya Afrika Mashariki ni miundo msingi ikiwemo reli na mabomba ya mafuta.