Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir
amelivunja bunge lake na kuunda serikali ya umoja, katika harakati za
kupiga jeki makubaliano ya amani yanayolenga kumaliza vita vya wenyewe
kwa wenyewe vya takriban miaka miwili.
Mpango huo unaowashirikisha waliokuwa waasi katika serikali ulitangazwa Alhamisi katika runinga ya taifa.Theluthi moja ya mawaziri wa bunge hilo jipya ni wanachama wa chama cha SPLM-IO kilichobuniwa na aliyekuwa kiongozi wa waasi Riek Machar,ambaye alirudi mjini Juba mapema wiki hii ili kuapishwa kuwa makamu wa kwanza wa rais.
Msemaji wa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa aliunga mkono hatua hiyo kama ya kihistoria katika makubaliano hayo ya amani.
Makumi ya maelfu wameuawa na watu milioni 2 wakiwachwa bila makao katika mgogoro huo wa Sudan Kusini ambayo ilipata uhuru wake mwaka 2011.