Recent Posts

PropellerAds

Friday, June 17, 2016

Auawa akichuma kuvu yenye 'nguvu za kiume'

Mtu mmoja amepigwa risasi na kuuawa katika kijiji cha Nepal alipokuwa akichuma kuvu fulani inayotambuliwa kwa uwezo wake wa kuongeza nguvu za kiume.
Kuvu hiyo inayotambulika kama ''Himalayan Viagra'' inasemekana kuwaongezea ashki walaji wake.
Kuvu hiyo ni kitega uchumi cha wenye vijiji wa maeneo ya milimani.
Haijulikani kwanini genge hilo la wavamizi liliwashambulia watu hao waliokuwa wakichuma kuvu hiyo katika wilaya ya mugu ila maafisa wa utawala wamethibitisha kuwa watu wengine watatu walijeruhiwa katika shambulizi hilo.
Ukungu au kuvu hiyo humea kwenye mwili wa nondo au mtoto wa kipepeo na kilo moja ya kuvu hiyo inaweza kuuza kwa maelfu ya dola za Marekani nchini Uchina.
Biashara hiyo ni mojawapo ya njia ambazo raia wengi masikini wa jamii zinazoishi katika maeneo ya milima ya Hilamaya hujipatia riziki.
Kila mwaka maelfu ya watu kutoka vijijini hufunga safari kwa kutumia nyumbu na ngombe hadi maeneo ya milimani kutafuta ukungu huo unaomea kwenye mwili wa nondo.
Wakati wa msimu wa mavuna, shule hata hufungwa ili wanafunzi wawasaidie wazazi wao kutafuta kuvu.
Hii sio mara ya kwanza kwa ghasia kutokea katika eneo hilo.
Mwaka wa 2009 watu saba waliuawa baada ya mzozo kutokea kuhusu hati miliki ya kutafuta ukungu huo katika maeneo ya milima.
Licha ya utajiri unaotokana na mauzo ya ukungu, raia wengi nchini humo wanaiona kuwepo kwake kama laana kubwa kwa jamii.