Recent Posts

PropellerAds

Wednesday, June 8, 2016

Bajeti ya Serikali 2016/ 2017 yawa kivutio cha watanzania.

Bajeti ya kwanza ya Serikali ya Awamu ya Tano
itaizidi ya Serikali ya Awamu ya Nne kwa Sh7.1 trilioni
baada ya Waziri wa Fedha kutangaza sura ya bajeti ya
mwaka 2016/17 inayoonyesha kutakuwa na makusanyo
na matumizi ya Sh29.5 trilioni.
Sura hiyo ya bajeti ya mwaka 2016/17 inatofautiana
na iliyopita iliyokuwa ya Sh22.45 trilioni katika maeneo
mengi, ikiwa ni pamoja na kiwango cha fedha
kitakachotengwa kwa ajili ya shughuli za maendeleo,
ambacho ni zaidi ya mara mbili ya fedha za eneo hilo
katika bajeti iliyopita.
Waziri wa Fedha, Dk Phillip Mpango alisema wakati
akiwasilisha mapendekezo ya kiwango cha ukomo wa
bajeti jijini Dar es Salaam jana kuwa kati ya fedha
hizo, Sh18.46 trilioni, ambazo ni sawa na asilimia 62.5
ya bajeti yote, zitatokana na jumla ya mapato ya ndani
yanayohusisha na halmashauri.
Kiwango hicho kimezidi Sh3.64 trilioni ya bajeti
iliyopita ambayo ililenga kukusanya Sh14.82 trilioni.
“Kati ya mapato hayo, Serikali inalenga kukusanya
mapato ya kodi ya jumla ya Sh15,105 bilioni, sawa na
asilimia 82 ya mapato ya ndani,” alisema Dk Mpango.
Alisema makisio ya mapato ya kodi na yasiyo ya kodi
yameongezeka kwa kuwa kuna viashiria vingi
vinavyoonyesha kwamba Mamlaka ya Mapato (TRA)
kwa kushirikiana na wizara na taasisi zinazokusanya
maduhuli, zina uwezo wa kukusanya kiasi hicho.
Alisema: “Kipaumbele cha kwanza cha Serikali kitakuwa
ni kujizatiti katika ukusanyaji wa mapato kwa kubuni
vyanzo vipya na kuendelea kudhibiti mianya mbalimbali
ya ukwepaji wa kodi. Suala hili linahitaji ushirikiano wa
karibu na wananchi ili tujiletee maendeleo ya haraka kwa
kushiriki kulipa kodi na kuwafichua wakwepa kodi kwa
kuwaona kama maadui wa maendeleo yetu.”
Kwa mujibu wa Dk Mpango, Sh17.72 trilioni zitakuwa
kwa ajili ya matumizi ya kawaida, wakati Sh11.82
trilioni, sawa na asilimia 40 ya bajeti nzima,
zimetengwa kwa ajili ya shughuli za maendeleo.
Katika bajeti iliyopita, matumizi ya kawaida
yalitengewa Sh16.7 trilioni, sawa na asilimia 74.3
wakati shughuli za maendeleo zilipangiwa Sh5.76
sawa na asilimia 25.9.
“Asilimia 40 kwenda kwenye mipango ya maendeleo, hili
ni jambo jema,” alisema Freeman Mbowe, ambaye ni
mwenyekiti wa Chadema na kiongozi wa kambi ya
upinzani bungeni, alipoongea na waandishi.
“Kwamba tumepunguza matumizi ya kawaida ya Serikali
na kuelekeza fedha zaidi kwenye mipango ya maendeleo,
nasema hili ni jambo jema kama litatekelezeka.”
Vipaumbele
Kwa mujibu wa Dk Mpango, shughuli zitakazopewa
kipaumbele kwenye mipango hiyo ya maendeleo
zimegawanywa katika maeneo manne ambayo ni
viwanda vya kukuza uchumi na ujenzi wa msingi wa
uchumi wa viwanda, kufungamanisha maendeleo ya
uchumi na rasilimali watu, mazingira wezeshi kwa
uendeshaji biashara na uwekezaji na pia usimamizi wa
utekelezaji wa mpango.
Dk Mpango alisema washirika wa maendeleo
wanatarajiwa kuchangia Sh3.6 trilioni, ikiwa ni
ongezeko la Sh1.7 trilioni kulinganisha na Sh1.88
trilioni zilizokuwa zinategemewa kwenye bajeti
iliyopita.
Fedha hizo zitakuwa za misaada na mikopo nafuu
kutoka nje ambayo ni pamoja na GBS, Basket Fund na
miradi ya maendeleo.
Aidha Serikali inatarajia kukopa Sh5,374.3 bilioni
kutoka soko la ndani kwa ajili ya kulipia hati fungani
na dhamana za Serikali zinazoiva pamoja, wakati
kutoka kwenye soko la nje kwa masharti ya kibiashara
inatarajia kukopa Sh2.1 trilioni.
Awali Spika Job Ndugai alisema kwa mujibu wa
utaratibu mapendezo hayo yalipaswa kuwasilishwa
tangu Machi 11, lakini kutokana na ratiba za wabunge
wengi kuwa kwenye majimbo yao, aliamua kuongeza
siku.
“ Sasa ninawashauri wabunge wote kwenda kuyasoma
mapendekezo hayo vyema ili mpate nafasi ya kuchangia
fedha bajeti itakapowasilishwa bungeni. Pia mhudhurie
kwenye vikao vya kamati zenu ili kujipanga vyema. Wale
watakaokuwa hawaonekani kwenye vikao, tutawasilisha
majina yao kwenye vyama vyao ili wachukuliwe hatua
zinazostahili.”
Miradi ya maendeleo
Katika kuongeza wigo wa makusanyo ya kodi, Dk
Mpango alisema sera za mapato kwa mwaka
2016/2017 itajielekeza kufanya tathimini ya mkupuo
ya majengo ili kuongeza mapato.
Katika mpango wa kuifanya Tanzania kuwa nchi ya
viwanda, Dk Mpango alisema kipaumbele kitakuwa ni
mradi wa magadi soda ulioko kwenye Bonde la
Engaruka ambako utafiti umebaini kuna magadi ya
mita za ujazo bilioni 4.68 ambazo huongezeka kila
mwaka kwa mita milioni 1.9 za ujazo.
“Mradi utahusisha kiwanda cha kuzalisha tani milioni
moja za magadi kwa mwaka kwa ajili ya matumizi ya
viwanda, hususan madawa, vioo na sabuni,” alisema.
Mradi huo utakapokamilika utaliingizia taifa Sh 400
bilioni kwa mwaka.
Eneo jingine ni kufufua kiwanda cha General Tyre cha
Arusha, ambacho kimetengewa Sh2 bilioni kwa kazi
hiyo. Pia kiwanda cha viuadudu kilichopo Kibaha
mkoani Pwani ambacho mradi wake utatekelezwa kwa
awamu tatu, mbili za mwisho zikihusisha ujenzi wa
kiwanda cha mbolea na cha virutubisho.
Pia mpango huo utahusisha uendelezaji wa viwanda
vidogo mkoani Morogoro, Dar es Salaam, Mbeya na
Mwanza.
Katika kufunganisha maendeleo ya uchumi na
rasilimali watu, Serikali itaweka nguvu kwenye elimu
na mafunzo ya ufundi, ikihusisha kuimarisha mifumo,
majengo na miundombinu katika shule za awali, msingi
na sekondari.
Pia itahusisha ukarabati, upanuzi na ujenzi wa vyuo
vikuu, mradi wa upanuzi wa Chuo Kikuu Kishiriki cha
Elimu (Mkwawa, Duce, Udom na OUT, Ardhi, Mzumbe,
Sokoine, Muhimbili, Ushirika, Chuo Kikuu cha Sayansi
cha Mwalimu Nyerere na pia mikopo ya wanafunzi wa
elimu ya juu.
Eneo hilo litahusisha uendelezaji ustawi wa jamii kwa
kuangalia huduma za afya, maji, kazi na ajira, na
uwezeshaji wananchi kwa kutoa Sh50 milioni kwa kila
kijiji.
Mazingira wezeshi
Katika kujenga mazingira wezeshi, Serikali itaongeza
uwezo wa uzalishaji umeme, usambazaji umeme mijini
na vijijini, ujenzi wa kiwanda cha kupokea, kuchakata
na kubadilisha gesi asilia kuwa katika kimiminika kwa
ajili ya kusafirisha nje, ujenzi wa miundombinu ya
kusafirisha gesi asilia, ujenzi wa miundombinu ya
usafiri, teknolojia ya habari na mawasiliano, miradi ya
makaa ya mawe na mradi wa chuma wa Liganga.