Recent Posts

PropellerAds

Monday, March 14, 2016

Chombo chatumwa kutafuta uhai Mars

Wataalamu wa anga za juu wa Ulaya kwa ushirikiano
na wenzao wa Urusi wamerusha angani chombo cha
anga za juu kitakachofanya utafiti kubaini iwapo kuna
uhai sayari ya Mirihi, kwa Kiingereza Mars.
Chombo hicho kwa jina ExoMars Trace Gas Orbiter
(TGO), kimepaa kutoka Baikonur nchini Kazakhstan
saa 09:31 GMT.
Chombo hicho kitafanya uchunguzi kubaini iwapo gesi ya
Methane ambayo imepatikana katika anga ya sayari hiyo
inatokana na shughuli ya kijiolojia au inatokana na
viumbe hai.
Mambo yote yakienda ilivyopangwa, wataalamu
wanapanga baadaye kurusha mtambo wa kusafiri juu ya
sayari, kwa kimombo rover, ambao utatumiwa kuchimba
chini ya ardhi ya Mars.
Mtambo huo, utaunganishiwa nchini Uingereza, unaweza
kurushwa mwaka 2018 au ukichelewa mwaka 2020.
Inakadiriwa kwamba itachukua roketi iliyobeba chombo
cha TGO saa 10 ili kujiweka kwenye njia sahihi ya
kuelekea sayari ya Mars.
Safari ya chombo hicho hadi Mars inatarajiwa kuchukua
miezi saba, na sehemu ya chombo kwa jina Schiaparelli
inatarajiwa kutua Mars tarehe 19 Oktoba. Sehemu ya
setilaiti ya chombo hicho itazunguka sayari hiyo
ikikusanya maelezo muhimu kuhusu hewa na gesi
zinazopatikana katika sayari hiyo.
Safari ya chombo hicho inafuatiliwa na wataalamu wa
Shirika la Anga za Juu la Ulaya mjini Darmstadt,
Ujerumani.
Mradi huo wa TGO ndio wa kwanza kabisa kufanywa
na Ulaya na Urusi kwa pamoja kuelekea sayari ya
Mars, ambayo ndiyo ya nne kutoka kwenye jua.
Uchunguzi wa awali wa setilaiti zinazozunguka dunia na
rover ya Curiosity ya Marekani umebaini kuwepo kwa
haidrokaboni ingawa za vipimo vya chini sana katika
sayari hiyo.
Moja ya mambo yanayoweza kuwa yanachangia kuwepo
kwa gesi hizo ni shughuli za kijiolojia ndani ya sayari
hiyo ambapo maji yanaweza kuwa yanachanganyikana na
mawe na kuzalisha gesi ya haidrojeni ambayo baadaye
inageuka na kuwa methane.
Jambo jingine linaloweza kuwa linasababisha kuwepo kwa
gesi hiyo ni kuwepo kwa viumbe hai.
Sehemu kubwa ya gesi ya methane duniani hutokana na
viumbe hai.