Recent Posts

PropellerAds

Friday, March 18, 2016

Raia wa Kenya waishitaki Tanzania

Raia kumi wa Kenya wameituhumu Serikali ya Tanzania,
kwa kuwateka jijini Maputo nchini Msumbiji Januari
2006, ambako walikuwa wakiishi kihalali wakitafuta
fursa za biashara, na kisha kuwapakiza kwenye ndege
ya kijeshi na kuwaleta nchini Tanzania kwa nguvu.
Kwa upande wake, serikali ya Tanzania kupitia mawakili
wake imepinga madai hayo na kuitaka Mahakama ya
Afrika ya Haki za Watu kutupilia mbali maombi ya
watuhumiwa.
Tanzania inasema watuhumiwa hao walikamatwa katika
uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere baada
ya kuletwa kupitia ndege ya jeshi la Msumbiji.
Wakenya hao wanahoji kuwa kesi yao nchini Tanzania
imechukua muda mrefu kwa kuahirishwa mara kwa mara
bila sababu.
Aidha wanadai kuwa kesi imeendeshwa bila wao kuwa
na mawakili wa kuwatetea.
Mawakili wa serikali ya Tanzania pia waliieleza
Mahakama ya Afrika kuwa, wawili kati ya raia hao wa
Kenya waliofariki wakiwa magereza, walikufa kwa kifo
cha kawaida, na kesi iliahirishwa mara kwa mara
kutokana na mawakili wa walalamishi kukosa kufika
mahakamani siku za kesi.
Wakenya hao walikamatwa miaka kumi iliyopita na
kuhukumia kufungwa miaka thelathini jela, baada ya
kukutwa na hatia ya kosa la mauaji na ujambazi wa
kutumia silaha lililofanyika katika benki ya NMB Tawi la
Moshi, mwezi Mei 2004.
Mahakama ya Africa kuhusu haki za binadamu na za
watu iliundwa mwaka 2006 na kuanza kazi zake rasmi
mwaka mmoja baadaye. Hadi kufikia mwishoni mwa
mwezi februari 2016, Mahakama imepokea kesi 74,
ambapo 25 kati ya hizo zimekwisha shughulikiwa, huku
kesi 4 zikipelekwa katika Tume ya Afrika ya Watu na
Haki za Binadamu nchini Gambia.