Jaji mmoja mzungu nchini Afrika
Kusini ameshutumiwa vikali baada ya kudaiwa kusema kwenye mitandao ya
kijamii kwamba ubakaji ni kawaida kwa wanaume weusi.
Jaji Mabel
Jansen alisema unajisi wa watoto na wasichana na pia ubakaji wa wanawake
ni jambo la “kufurahiwa” la kupitisha wakati miongoni mwa Waafrika.Kadhalika, amenukuliwa pia akisema hajawahi kukutana na msichana mweusi ambaye hajawahi kubakwa.
Kampeni imeanzishwa ya kutaka afutwe kazi.
Akijitetea, jaji huyo amesema amefasiriwa vibaya na kwamba matamshi hayo yametumiwa vibaya nje ya muktadha.
Jaji Jansen anadaiwa kutoa matamshi hayo kwenye mawasiliano na mwanaharakati Gillian Schutte kwenye Facebook mwaka jana lakini yamesambazwa sana wikendi.
"Katika utamaduni wao, mwanamke yuko hapo kuwaburudisha. Mwisho. Hutazamwa kama haki yao na mtu hatakiwi kuomba ruhusa kutoka kwa mwanamke,” jaji huyo amenukuliwa akisema.
Wakili mashuhuri Afrika Kusini Vuyani Ngalwana amesema matamshi hayo ya jaji huyo yanawaharibia sifa wanaume wote weusi na kuwaonesha kama wabakaji.
Amesema ni ya kushangaza sana, kwa mujibu wa gazeti la Business Day.
Bw Ngalwana amesema Tume ya Huduma za Mahakama inafaa kumtaka afafanue matamshi hayo kabla ya kumchukulia hatua.
Msemaji wa chama tawala cha African National Congress (ANC) amesema anashuku kuna majaji wengi wenye mtazamo wa kibaguzi.
Utawala wa Wazungu ambao ulihalalisha ubaguzi wa rangi ulifikia kikomo nchini Afrika Kusini mwaka 1994.