Kundi la watu wanaojidai kuwa
wapiganaji wa Kiislamu limeweka video mtandaoni likidai uwepo wa wa
wapiganaji wa Kiislamu nchini humo.
Video hiyo inawaonesha wanaume hao wakiwa wamejifunika nyuso zao kwa vitambaa na barakoa.Wanadai wamo katika mji wa Tanga na kuwahimiza Waislamu katika taifa hilo la Afrika Mashariki kujiunga na kampeni yao.
Ukurasa wa Twitter ambao unasambaza video hiyo ya dakika tano unasema wanaume hao ni tawi la Afrika Mashariki la kundi linalojiita Islamic State (IS).
Mwandishi wa BBC anayeangazia masuala ya usalama Afrika, Tomi Oladipo, anasema hakuna ushahidi wa uhusiano wa moja kwa moja kati ya wapiganaji hao na kundi la Islamic State.
Serikali ya Tanzania imesema inafahamu uwepo wa video hiyo pamoja na ujumbe uliochapishwa kwenye Twitter na inafanya uchunguzi kubaini uhalisi wake.
Waziri wa mambo ya ndani Charles Kitwanga ameambia BBC kwa njia ya simu kwamba serikali inachukulia habari hizo kwa uzito akisema zinaweza kutishia usalama wa taifa.