Mji mmoja nchini Uzbekistan umekua
ukiwapa waalimu wake kuku kama mshahara badala ya pesa. Mamlaka za mji
wa Nukus katika jimbo linalojitawala la Karakalpakstan wamekua wakitia
vifaranga wachanga kwa walimu kutokana na uhaba wa pesa nchini humo.
Kituo
cha radio kinachofadhiliwa na Marekani{Radio Ozodlik} kimemnukuu
mwalimu mmoja akilaani hatua hiyo kama aibu kubwa kwa mamlaka.Mwalimu huyo aliyeghadhabishwa na hatua hiyo amesema hataki vifaranga kwa sababu anaweza kuwapata sokoni, lakini wanataka pesa zao.
Vifaranga wanaotolewa kama mshahara wana gharama ya dola mbili kila mmoja, ikiwa ni maradufu bei inayouzwa vifaranga sokoni.
Mamlaka za Uzbekistan hazikubalii uhuru wa vyombo vya habari na raia wa huko hutegemea vyombo vya habari vya kimataifa kutoa sauti yao, ila hawajitambulishi.
Uzbekistan imekumbwa na uhaba wa fedha kwa miaka sasa hali inayosababisha serikali kuchelewesha mishahara ya wafanyikazi na malipo ya uzeeni.
Mapema mwezi huu wafanyikazi wa serikali katika mji mkuu,Tashkent walilalamikia kwamba hawakuwa wamelipwa mshahara kwa miezi miwili kwa sababu benki hazikuwa na pesa.